Quantcast
Channel: Gospel Kitaa™
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1245

MWANASHERIA MKUU WA ZANZIBAR AFUTWA KAZI

$
0
0
Aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Zanzibar,  Mhe. Othman Masoud Othman, akipiga kura kwenye Bunge Maalum la Katiba, Oktoba 1, 2014
RAIS wa Zanzibar na Mweneyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein amemteua Mh. Said Hassan Said kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi Dkt.Abdulhamid Yahya Mzee, Dkt Shein amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu 55(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Mheshimiwa Said Hassan anachukua nafasi ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman ambaye Uteuzi wake umefutwa kwa mujibu wa Vifungu vya 53, 54 (1) na 55 (3) vya Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Kifungu 12(3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya 2011.

Kabla ya Uteuzi huo Mheshimiwa Said Hassan Said alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Uteuzi huo umeanza tarehe 07, Oktoba, 2014

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 07, Oktoba, 2014

Mhe. Othman Masoud Othman akiondolewa Bungeni na maafisa usalama ili kumnusuru kwa lolote baya, ambapo wajumbe wenzake kutka Visiwani Zanzibar walimcharukia kwa kupiga kura ya hapana kwa baadhi ya vifungu.
Kura ya Hapana alipokuwa kwenye Bunge Maalum
Mwandishi mkongwe na mwanasheria, Ally Saleh, kupitia tovuti ya Mzalendo, aliweka vifungu ambavyo mwanasheria mkuu wa Zanzibar alivikataa wakati wa upigaji wa kura kwenye Bunge Maalum la Katiba, jambo lililoibua sintofahamu kwa wajumbe wengi kutoka visiwani humo, wengine wakimtaka Rais Shein amfukuze kazi. Ni vema ukafahamu vipengele alivyovikataa waziwazi pasi mashaka.

___
Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 
2.-(1) Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni:
(a) eneo lote la Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na eneo lake la bahari ambalo kabla ya Muungano lilikuwa likiitwa Jamhuri ya Tanganyika pamoja na maeneo mengine yatakayoongezeka; na
(b) eneo lote la Zanzibar, ikiwa ni pamoja na eneo lake la bahari ambalo kabla ya Muungano lilikuwa likiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar pamoja na maeneo mengine yatakayoongezeka.
(2) Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine na kwa upande wa Zanzibar, Rais anaweza kukasimu mamlaka hayo kwa Rais wa Zanzibar.
(3) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), Bunge litatunga sheria itakayoainisha na kufafanua mipaka ya eneo la Jamhuri ya Muungano.
——–
Ukuu na utii wa Katiba

9.-(1) Katiba hii ni sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba hii.
(2) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), endapo masharti ya sheria yoyote itakayotungwa na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria yatatofautiana na masharti ya Katiba hii, masharti ya sheria hiyo yatakuwa batili na yatatenguka kwa kiwango kile kinachotofautiana na masharti ya Katiba hii.
(3) Mtu yeyote, chombo au taasisi ya Serikali, jumuiya, wakala yeyote
na mamlaka binafsi zitakuwa na wajibu wa kuzingatia na kutii masharti ya
Katiba hii na sheria za nchi.
(4) Sheria yoyote, mila, desturi au uamuzi wowote wa chombo cha dola
au ofisa wa Serikali ni sharti ufuate na kuzingatia masharti yaliyomo kwenye Katiba hii na kwamba sheria, mila, desturi au uamuzi wowote ambao hautawiana au kwenda sambamba na masharti ya Katiba hii utakuwa batili.
(5) Serikali itaweka utaratibu wa kuwawezesha wananchi kuifahamu, kuilinda na kuitii Katiba hii.
——-
Muundo wa Muungano

70. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa Serikali mbili ambazo ni:
(a) Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na
(b) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
——–
Utekelezaji wa shughuli za Mamlaka ya Nchi

71.-(1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano
zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya utoaji haki, na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.
(2) Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; vyombo vyenye mamlaka ya utoaji haki vitakuwa ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama Kuu ya Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.
(3) Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa katika Ibara hii, kutakuwa na Mambo ya Muungano kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba hii na pia kutakuwa na mambo yasiyo ya Muungano, ambayo ni mambo mengine yote yasiyo ya Muungano.
(4) Kila chombo kilichotajwa katika Ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake kwa kufuata masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii.
——-
Mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano

72. Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya utekelezaji katika Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano na kwa mambo yote yasiyo ya Muungano yanayohusu Tanzania Bara.
——
Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano

73.-(1) Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na mamlaka na haki juu ya mambo yasiyo ya Muungano yanayohusu Zanzibar.
(2) Bila kuathiri mipaka iliyowekwa na Katiba hii, katika kutekeleza mamlaka yake chini ya ibara ndogo ya (1), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa na uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa.
(3) Endapo, katika kutekeleza mamlaka na majukumu yake kwa mujibu wa Ibara hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahitaji kupata ushirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kufanikisha uhusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi ya kikanda au kimataifa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza kufanikisha uhusiano au ushirikiano huo kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii na sheria itakayotungwa na Bunge.
(4) Kwa madhumuni ya Ibara hii, Bunge litatunga sheria itakayoainisha
na kufafanua:
(a) majukumu na mipaka ya utekelezaji wa mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;
(b) utaratibu wa kushughulikia athari zinazotokana na uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;
(c) utaratibu wa utafutaji na upatikanaji wa mikopo na misaada kutokana na uhusiano au ushirikano huo;
(d) utaratibu au masharti ya kuvunja au kuimarisha uhusiano au ushirikiano huo;
(e) utaratibu wa mawasiliano na mashauriano kati ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa;
(f) utaratibu wa utekelezaji wa masharti ya Ibara hii; na
(g) mambo mengine yatakayohusu uhusiano au ushirikiano wa kikanda au kimataifa chini ya Ibara hii.
———
Mahusiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar

74.-(1) Katika kutekeleza majukumu yake katika maeneo mbalimbali, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itazingatia misingi ya kushirikiana na kushauriana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la Zanzibar kukuza na kulinda maslahi ya Taifa na maendeleo ya wananchi.
(2) Kwa madhumuni ya kukuza umoja na uhusiano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, zinaweza kushauriana na kushirikiana katika mambo yanayohusu uongozi, utawala, vyombo vya uwakilishi na mahakama.
(3) Utendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au chombo chochote cha Serikali hizo utatekelezwa kwa kuzingatia umoja wa Jamhuri ya Muungano na wajibu wa kukuza utaifa.
(4) Bila kuathiri masharti ya Ibara hii, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano maalum baina yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaweza kutekeleza jambo lolote lililo chini ya mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mujibu wa makubaliano hayo.
———
Wajibu wa viongozi wakuu kulinda Muungano

75.-(1) Bila kuathiri wajibu wa kila raia uliotajwa katika Katiba hii, kila kiongozi mkuu mwenye mamlaka ya utendaji katika Jamhuri ya Muungano aliyetajwa katika ibara ndogo ya (3) atakuwa na wajibu, katika kutekeleza madaraka aliyopewa kwa mujibu wa Katiba hii, kuhakikisha kuwa anatetea, analinda, anaimarisha na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(2) Kwa madhumuni ya masharti ya ibara ndogo ya (1) kila kiongozi
mkuu aliyetajwa katika ibara ndogo ya (3), kabla ya kushika madaraka yake, ataapa kuutetea, kuulinda na kuudumisha Muungano kwa mujibu wa Katiba hii.
(3) Viongozi wakuu wanaohusika na masharti ya Ibara hii ni:
(a) Rais wa Jamhuri ya Muungano;
(b) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano;
(c) Rais wa Zanzibar;
(d) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano; na
(e) Makamu wa Rais wa Zanzibar.
——–
Utaratibu wa uchaguzi wa Rais
86.-(1) Katika uchaguzi wa Rais kila chama cha siasa kitakachotaka kushiriki katika uchaguzi wa Rais, kitawasilisha kwa Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano, kwa mujibu wa sheria, jina la
mwanachama mmoja anayependekezwa kwa nafasi ya madaraka ya Rais.
(2) Endapo ni mgombea huru, kwa kuzingatia sifa zitakazoainishwa
katika sheria itakayotungwa na Bunge atawasilisha jina lake kwenye Tume Huru ya Uchaguzi.
(3) Mapendekezo ya majina ya wagombea katika uchaguzi wa Rais yatawasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi katika siku na kwa utaratibu
utakaoainishwa katika sheria.
(4) Endapo itafika siku na saa iliyotajwa kwa ajili ya
kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wagombea, ni mgombea mmoja tu
ambaye anapendekezwa kuwa halali, Tume Huru ya Uchaguzi itawasilisha jina lake kwa wananchi, nao watapiga kura ya kumkubali au kumkataa kwa mujibu wa masharti yaliyoainishwa katika Katiba hii na sheria.
(5) Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano utafanyika siku itakayoteuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
(6) Mgombea wa nafasi ya madaraka ya Rais atatangazwa kuwa
amechaguliwa kuwa Rais iwapo atapata kura zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote halali zilizopigwa kwa nafasi ya madaraka ya Rais.
(7) Endapo katika uchaguzi wa Rais hakuna mgombea aliyekidhi masharti ya ibara ndogo ya (6), basi uchaguzi utarudiwa ndani ya siku sitini kwa wagombea walioshika nafasi ya kwanza na ya pili na mgombea atakayepata kura zaidi ya asilimia hamsini atatangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais.
(8) Mambo mengine yote yahusuyo utaratibu wa uchaguzi wa Rais yatakuwa kama itakavyofafanuliwa katika sheria itakayotungwa na Bunge kwa ajili hiyo.
———
Madaraka ya kutunga Sheria

128.-(1) Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Bunge.
(2) Mamlaka yoyote ya kutunga sheria katika Zanzibar juu ya mambo
yote yasiyo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.
(3) Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu
jambo lolote katika Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka na pia endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka.
(4) Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote haitatumika Zanzibar isipokuwa kwa mujibu wa masharti yafuatayo:
(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vilevile Zanzibar au iwe inabadilisha, kurekebisha au kufuta sheria inayotumika Zanzibar;
(b) Sheria hiyo iwe inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria iliyokuwa inatumika tangu zamani Tanzania Bara ambayo ilikuwa inatumika pia Zanzibar kwa mujibu wa Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ya mwaka 1964, au kwa mujibu wa sheria yoyote ambayo ilitamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara navilevile Zanzibar; au
(c) Sheria hiyo iwe inahusu Mambo ya Muungano, na kila inapotajwa Tanzania katika Sheria yoyote ifahamike kuwa sheria hiyo itatumika katika Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na masharti ya Ibara hii.
(5) Bila kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba hii kuhusu mambo yote ya Zanzibar yasiyo Mambo ya Muungano, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili.
———
Utaratibu wa kubadilisha Katiba
129.-(1) Bunge linaweza kutunga sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata kanuni zifuatazo:
(a) Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti ya Katiba hii au masharti yoyote ya sheria yanayohusu jambo lolote isipokuwa mambo yanayohusu aya ya (b) au (c), utapitishwa kwa kuungwa mkono kwa
wingi wa kura za Wabunge wote;
(b) Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Nyongeza ya Pili, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote wa Zanzibar;
(c) Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Nyongeza ya Tatu iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wananchi wa Tanzania Bara, na zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wananchi wa Tanzania Zanzibar katika kura ya maoni itakayoendeshwa na kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria.
(2) Kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (1) kubadilisha masharti ya Katiba hii maana yake ni pamoja na kurekebisha au kusahihisha masharti haya au kufuta na kuweka masharti mengine badala yake au kusisitiza au kubadilisha matumizi ya masharti hayo.
——–
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mamlaka yake

158.-(1) Kutakuwa na Serikali ya Zanzibar itakayojulikana kama “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar” ambayo itakuwa na mamlaka katika Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
(2) Bila kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii na katika ibara zifuatazo katika Sura hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaundwa na kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na Katiba ya Zanzibar ya 1984.
——
Rais wa Zanzibar na mamlaka yake

159.-(1) Kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar atakayechaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984.
(2) Rais wa Zanzibar kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Jaji Mkuu wa Zanzibar kiapo cha kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano, na kiapo kingine chochote kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kinachohusika na utendaji wa kazi yake, kisha atashika na kutekeleza madaraka hayo kwa mujibu wa Katiba hii na Katiba ya Zanzibar ya 1984.
——-
Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na kazi Zake

160.-(1) Kutakuwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar litakalokuwa na wajumbe wa aina na idadi itakayowekwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Zanzibar ya 1984.
(2) Bila kuathiri madaraka ya Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kama Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi litakuwa ndicho chombo kikuu cha kumsaidia na kumshauri Rais wa Zanzibar katika masuala ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuratibu utekelezaji wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na pia utekelezaji wa madaraka yake juu ya shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu mambo yote yasiyo Mambo ya Muungano,
——-
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar

161.-(1) Kutakuwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kama litakavyoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984.
(2) Madaraka yote ya kutunga sheria katika Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo Mambo ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
——–
Misingi ya matumizi ya fedha za umma
243. Misingi ifuatayo itaongoza matumizi ya fedha za umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania:
(a) fedha za umma zitatumika kwa uwazi, umakini na kwa uwajibikaji pamoja na kuzingatia ushiriki wa wananchi kupitia wawakilishi wao;
(b) mfumo wa fedha za umma utalenga kuwepo kwa:
(i) utozwaji kodi usio wa upendeleo au ubaguzi;
(ii) bajeti ya Serikali inayoweka vipaumbele kwa makundi na maeneo yaliyo nyuma kimaendeleo;
(c) matumizi ya rasilimali na mikopo ya Taifa yatazingatia ustawi linganifu kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo; na
(d) taarifa za usimamizi wa fedha za umma zitatolewa katika lugha inayoeleweka kwa wananchi.
——-
Akaunti ya Fedha
ya Pamoja
244. Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza akaunti maalum
itakayoitwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” na ambayo itakuwa ni sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambamo
kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa kiasi
kitakachoamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa sheria
itakayotungwa na Bunge, kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano.
——-
Tume ya Pamoja ya Fedha

245.-(1) Kutakuwa na Tume ya Pamoja ya Fedha yenye Wajumbe wasiozidi saba watakaoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar ambapo wajumbe watatu watatoka Zanzibar na wajumbe wanne watatoka Tanzania Bara.
(2) Majukumu ya Tume ya Pamoja ya Fedha yatakuwa ni:
(a) kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na, au yanayohusu utekelezaji wa mambo ya Muungano na kutoa mapendekezo kwa Serikali zote mbili kuhusu mchango na mgawo wa kila mojawapo ya
Serikali hizo;
(b) kuchunguza kwa wakati wote mfumo wa shughuli za fedha wa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali hizo mbili; na
(c) kutekeleza majukumu mengine ambayo Rais ataipatia Tume au kama Rais atakavyoagiza, na kwa mujibu wa sheria itakayotungwa na Bunge.
(3) Kwa madhumuni ya Ibara hii, Bunge litatunga sheria itakayoainisha
na kufafanua:
(a) masharti na taratibu za utekelezaji wa majukumu;
(b) masharti kuhusu wajumbe wa Tume;
(c) muundo na majukumu ya Sekretarieti;
(d) taratibu za uwasilishaji wa taarifa za Akaunti ya Pamoja ya Fedha na taarifa nyingine za Tume kuhusu utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa Katiba hii; na
(e) mambo mengine yote yanayohusu Tume ya Pamoja ya Fedha.
—–
Mfuko Mkuu wa Hazina

246. Kutakuwa na Mfuko Mkuu wa Hazina wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano utakaoitwa “Mfuko Mkuu wa Hazina” ambamo fedha zote zitakazopatikana kwa njia mbalimbali zitawekwa, isipokuwa:
(a) fedha ambazo zimetajwa katika sheria kuwa zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe katika mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum; au
(b) fedha ambazo kwa mujibu wa sheria, taasisi za Serikali zimeruhusiwa
kukusanya na kubaki nazo kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa taasisi hizo.
——
Masharti ya kutoa fedha za matumizi katika Mfuko Mkuu wa Hazina

247.-(1) Fedha zinaweza kutolewa kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina kwa ajili ya matumizi, kwa kuzingatia masharti yafuatayo:
(a) fedha hizo ziwe kwa ajili ya matumizi ambayo yameidhinishwa kuwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina na idhini hiyo iwe imetolewa kwa mujibu wa Katiba hii au sheria; na
(b) fedha hizo ziwe kwa ajili ya matumizi ambayo yameidhinishwa na sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali itakayotungwa mahsusi na Bunge au sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge.
(2) Kwa kuzingatia masharti ya ibara ndogo ya (1), fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina zitatolewa kutoka Mfuko huo kwa ajili ya matumizi kwa kuzingatia masharti kuwa matumizi hayo yawe yameidhinishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
(3) Fedha zilizomo katika mfuko maalum wowote wa Serikali, isipokuwa Mfuko Mkuu wa Hazina, hazitatolewa kutoka mfuko huo kwa ajili ya matumizi isipokuwa kwa mujibu wa sheria inayoidhinisha matumizi hayo.
——
Utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina

248.-(1) Rais atatoa maagizo kwa watu wanaohusika watayarishe na kuwasilisha kwenye Bunge, katika kila mwaka wa fedha wa Serikali, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha mwaka wa fedha wa Serikali unaofuata.
(2) Makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaliyotayarishwa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (1), yatawasilishwa kwanza kwenye Kamati husika ya Bunge kwa ajili ya kufanyiwa tathimini na uchambuzi.
(3) Kamati ya Bunge iliyopelekewa makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mujibu wa ibara ndogo ya (2), yaweza kukaribisha na kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu makadirio hayo, na baada ya kukamilisha tathmini na uchambuzi wa mapato na matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Kamati itaandaa taarifa yake kuhusu makadirio ya Serikali na kisha kuiwasilisha Bungeni.
(4) Baada ya Bunge kujadili na kuyakubali makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali yaliyowasilishwa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (1),
Serikali itawasilisha kwenye Bunge muswada wa sheria unaohusu matumizi ya fedha ya Serikali, kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina zitakazogharamia shughuli mbalimbali za Serikali zinazohusu makadirio hayo.
(5) Ikiwa katika mwaka wa fedha wowote inaonekana kwamba:
(a) fedha za matumizi zilizoidhinishwa na sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali kwa ajili ya kugharamia shughuli mahsusi hazitoshi;
(b) imekuwa lazima kulipa gharama za shughuli ambayo haikupangiwa fedha za matumizi kwa mujibu wa sheria za nchi;
(c) kuna fedha ambazo zimetumiwa kwa ajili ya shughuli mahsusi kwa kiasi kinachozidi kiwango cha matumizi kilichoidhinishwa na sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali kuhusu shughuli hiyo; au
(d) fedha zimetumiwa kulipia gharama za shughuli ambayo haikupangiwa fedha za matumizi kwa mujibu wa sheria za nchi, kutawasilishwa kwenye Bunge makadirio ya matumizi ya nyongeza au, kadri itakavyokuwa, maelezo ya matumizi ya ziada, na baada ya Bunge kuyakubali makadirio ya matumizi ya nyongeza au maelezo ya matumizi ya ziada, kutawasilishwa kwenye Bunge muswada wa sheria ya matumizi ya fedha ya Serikali au muswada wa sheria unaohusu matumizi ya nyongeza ya fedha ya Serikali kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina, na fedha hizo zitagharamia shughuli zinazohusika na makadirio au maelezo hayo.
——-
Utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha kabla ya sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali kuanza
kutumika

249.-(1) Iwapo mwaka wa fedha wa Serikali umeanza na sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali inayohusika na mwaka huo haijaanza kutumika, Rais anaweza kuidhinisha fedha zitolewe kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina kwa ajili ya kugharamia shughuli za lazima za Serikali, na fedha hizo zitatumiwa ndani ya miezi minne tangu mwanzo wa mwaka wa fedha wa Serikali au hadi sheria inayohusu matumizi ya fedha ya Serikali itakapoanza kutumika, kutegemea ni lipi kati ya mambo hayo litatangulia kutokea.
(2) Bunge litatunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina kwa kufuata utaratibu ulioelezwa katika ibara ndogo ya (1).
——
Mfuko wa Matumizi ya Dharura

250.-(1) Kutakuwa na Mfuko wa Matumizi ya Dharura ambao matumizi yake yatawekewa masharti katika sheria.
(2) Sheria iliyotajwa katika ibara ndogo ya (1) itaruhusu Rais au Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, pale anaporidhika kuwa kuna:
(a) jambo la haraka na la dharura na ambalo halikutazamiwa kutokea na ambalo halikupangiwa fedha, kuazima fedha kutoka Mfuko wa Matumizi ya Dharura kwa ajili ya kugharamia jambo hilo;
au
(b) jambo la haraka na la dharura kama ilivyoelezwa katika aya ya (a) ya ibara ndogo ya (2), kutumia fedha zilizotengwa mahsusi kwa ajili ya kugharamia shughuli fulani kulipia gharama za jambo hilo.
(3) Iwapo fedha zimeazimwa kutoka Mfuko wa Matumizi ya Dharura au fedha zilizotengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli fulani zimetumiwa kugharamia jambo la haraka na la dharura, basi kutawasilishwa kwenye Bunge makadirio ya matumizi ya nyongeza, na baada ya Bunge kuyakubali makadirio hayo muswada wa sheria unaohusu matumizi ya fedha za Serikali utakaowasilishwa kwenye Bunge kwa ajili ya kuidhinisha matumizi hayo utahakikisha kwamba fedha zozote zilizoazimwa kwenye Mfuko wa Matumizi ya Dharura zitarudishwa kwenye Mfuko huo kutoka katika fedha za matumizi yatakayoidhinishwa na muswada huo.
—–
Mishahara ya baadhi ya watumishi kudhaminiwa na Mfuko Mkuu wa Hazina

251.-(1) Kutakuwa na watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambao watalipwa mishahara na posho kama itakavyoelezwa na sheria.
(2) Kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (1), fedha za malipo ya mishahara na posho za watumishi wa Serikali wanaohusika na masharti ya Ibara hii pamoja na fedha za malipo ya uzeeni na kiinua mgongo, zitatolewa kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina.
(3) Mshahara anaolipwa mtumishi wa Serikali anayehusika na
masharti ya Ibara hii pamoja na masharti yake ya kazi havitabadilishwa kwa jinsi ambayo itapunguza maslahi ya mtumishi huyo baada ya kuteuliwa, isipokuwa kwamba masharti haya hayahusiki na posho anayolipwa mtumishi huyo.
(4) Endapo mtumishi wa Serikali anayehusika na masharti ya Ibara hii ana hiyari ya kuchagua kima cha mshahara au aina ya masharti ya kazi, basi kwa madhumuni ya ufafanuzi wa masharti ya ibara ndogo ya (3), mshahara wa kima hicho atakaochagua na aina hiyo ya masharti ya kazi atakayochagua vitahesabiwa kuwa vina maslahi zaidi kwake kuliko kima cha mshahara kingine chochote ambacho anaweza kuchagua au aina ya masharti ya kazi nyingine yoyote ambayo angeweza kuchagua.
(5) Masharti ya Ibara hii yatatumika kwa Jaji wa Mahakama ya Juu, Jaji
wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na watumishi wengine watakaoainishwa katika sheria za nchi.
——-
 
NYONGEZA YA KWANZA
______________
(Imetajwa katika Ibara ya 71(3))
Mambo ya Muungano
1. Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
3. Usalama na usafiri wa anga.
4. Uraia na uhamiaji.
5. Jeshi la Polisi.
6. Sarafu na Benki Kuu.
7. Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na Mashirika, ushuru wa forodha na ushuru
wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania na zinazosimamiwa na Idara ya Forodha.
8. Mambo ya nje.
9. Usajili wa vyama vya siasa.
10. Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani.
11. Elimu ya Juu.
12. Baraza la Taifa la Mitihani na mambo yote yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
13. Utabiri wa hali ya hewa.
14. Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 1245

Latest Images

Trending Articles

<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>