NENO LA LEO
"Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yako yote, na kuwa na afya yako kama roho yako ifanikiwavyo"
(3Yohana 1:2).
Mambo ya kujifunza:
1. "Mpenzi ninaomba..."
* Yesu anatuombea sisi.
Ni raha iliyoje kujua kuwa mbali ya "majukumu mengi" aliyonayo Bwana Yesu lakini bado anatuombea!
Sisi wanadamu hatuna mambo mengi kama Yesu lakini kwakweli ni ngumu mno kuombeana.
Maandiko mengine yanayotuonyesha kuwa Bwana Yesu anatuombea;
Waebrania 7:25, Warumi 8:32-34, 1Yoh 2:1-2
2. "Ufanikiwe katika mambo yako yote..."
Yesu Kristo (Mungu) anataka ufanikiwe KATIKA MAMBO YOTE.
Kujua tu kuwa "Mungu anafurahia mafanikio yako kwenye maeneo yote" itakufanya uombe kwa ujasiri, itakufanya uombe bila mashaka, itakufanya ubadili mtazamo wako kuhusu Maombi na mapenzi yake kwako, Itakufanya utarajie mambo makubwa na mazuri toka kwa Mungu kila siku!
Maandiko mengine yanayotuonesha kuwa Mungu anataka tufanikiwe;
Zaburi 1:1-3, Yeremia 17:5-8, Ayubu 36:11.
"Mungu anataka ufanikiwe katika kila jambo"
3. "...na kuwa na afya yako..."
Mungu anataka na anakuombea uwe na afya nzuri kila siku.
Mungu hafurahii kukuona unaumwa na kuugua kila siku.
Mungu anataka ufike mahali magonjwa yasiweze kabisa kukusumbua.
Mwili wako ni hekalu la Mungu.
Ni makao ya Roho wake mtakatifu, Mungu hataki uugue maana mwili wako ni hekalu na makao yake.
Ndio maana anaitwa Jehova Rapha yaani Mungu akuponyae (Kutoka 15:26), Ndio maana huwa analituma Neno lake ili kukuponya na kukutoa kwenye maangamizo (Zaburi 107:20), Ndiyo maana alimwaga damu yake msalabani na kukubali kupigwa ili "kwa kupigwa kwake wewe uponywe" kwa nguvu kubwa ya damu yake (1Petro 2:24), Amekusamehe dhambi zako zote ili apate "uhalali kisheria" wa kukuponya magonjwa yako yote (Zaburi 103:3).
Maandiko mengine kuonesha kuwa Mungu anataka uwe na afya nzuri na kukaa katika uzima wa kiafya;
Isaya 35:8-10, Mathayo 8:1-3, Mathayo 8:16-17.
"Mungu anataka usiteseke na magonjwa"
4. "...kama roho yako ifanikiwavyo"
Mungu ana kila kitu unachokihitaji lakini hatakupa chochote mpaka ahakikishe "umefanikiwa kiroho" yaani "umekua kiroho"!
Mungu huwa hatoi vitu vyake kwa "watoto wadogo" bali kwa "waliokua" (Wagalagia 4:1-3).
Mungu anataka ukue kiroho ili aweze kukubariki na kukustawisha.
Anataka "umjue sana" ili "mema yakujie na uwe na amani isiyovurugwa na chochote" (Ayubu 22:28).
Mungu anataka "umjue sana" ili akutumie kufanya mambo makuu (Danieli 11:32b).
Hivyo basi "kama watoto wadogo yatamanini maziwa ya akili yasiyogoshiwa (yasiyochanganywa maji) ili mpate KUUKULIA WOKOVU" (1Petro 2:2-6).
Hakikisha unakua kwenye wokovu/ maisha ya kiroho ili Mungu akupe baraka alizonazo.
Usipokazana kukua kiroho, utaishia kulaumu kwamba hujaona wema wa Mungu na baraka zake.
"Onja uone ya kuwa Yesu ni mwema" (Zaburi 34:8).
Muhimu: Jitahidi hakikisha umeyasoma maandiko yote haya leo.
Usiwe Mkristo shabiki asiyesoma Neno la Mungu.