(II) MAOMBI YA SIFA NA KUABUDU.
Bwana Yesu asifiwe…
Sifa na kuabudu ni mojawapo ya aina ya maombi ambapo mwombaji hutumia muda wake kusifu na kuabudu jina la Bwana katika uzuri na utakatifu kwa msaada wa Roho mtakatifu. Ikumbukwe kwamba sifa na kuabudu ni sehemu ya ibada.
Tena MUNGU hupendezwa na ibada ya namna hii ikiwa inatoka rohoni na kweli,maana biblia inasema Yeye huketi juu ya sifa;“Na Wewe U Mtakatifu,Uketiye juu ya sifa za Israeli.” Zab.22:3. Hivyo basi, sifa na kuabudu ni sehemu ya maombi kwa sababu kwa njia ya kusifu na kuabudu tunazungumza na Mungu labda waweza kusema kivipi? Ni hivi;
Tunaposifu na kuabudu katika roho na kweli iwe ni kwa njia ya kuimba au kunena sifa za Bwana,tunakuwa tukiwasiliana kwa ukaribu na Mungu wetu na mawasiliano ya namna hii yana nguvu ya ajabu ambapo BWANA MUNGU hushuka na kukutana na mahitaji yetu,mara nyingine hata tusipoomba matakwa yetu,Yeye huweka majibu. Hili nikuambialo hapa ni kweli na amin,jaribu kufanya hivyo kisha utaona milango ya mambo yako ikifunguka.
Si wengi wenye kuijua siri hii kwamba sifa na kuabudu ni sehemu ya maombi yenye nguvu sana. Kwa maana kuna kipindi hatuitaji kuomba~omba mambo yetu binafsi yaani isiwe kila siku uombapo, uombe “Baba naomba…” “Baba naomba…” bali kuna kipindi yatupasa kumsifu na kumuabudu Bwana katika Roho na kweli tu.
Bwana hutushindia vita na watesi wetu pale tunapokaza kumsifu Yeye katika Roho na kweli. Fikiria ; upo katika vita kali,labda adui yako amekuinukia kiasi kwamba umekosa msaada kwa ndugu zako hata rafiki zako wamekutenga, lakini ukaanza kumgeukia Mungu huku ukimuinua na kumtukuza ukisema;
“Wewe ni Mungu,Bwana wa vita,Mungu mzuri,mwenye nguvu ninakuabudu…. hata kwa hili ninalopitia sasa,bado wanipenda ninakuabudu Eeh Bwana Yesu,pokea sifa na utukufu maana wastahili….N.K” Je katika sifa zote hizi, BWANA hatakufanyia mlango wa kutokea katika hilo jaribu?
Jibu ni jepesi kabisa, ni Kweli Bwana atakupigania tu,kwa maana ulimuabudu katika roho na kweli. Labda nikuoneshe hili kibiblia, tunajua habari za wana wa Yuda chini ya utawala wa Yehoshafati kipindi ambacho waliinukiwa na mataifa matatu yenye nguvu. Mataifa hayo yalikuwa wana wa Moabu,wana wa Amoni na pamoja nao baadhi ya Wameuni(Waamoni). Watu hawa walikuja kupigana na watu wa Yuda chini ya utawala wake Yehoshafati.
Akini Yehoshafati,baada ya kuutafuta uso wa Mungu kisha wakaenda vitani,panapo majira ya vita,Yehoshafati akawaweka watu watakaomwimbia BWANA mbele ya jeshi lake. Kumbuka; akina Yehoshafati hawakuwa na uwezo wa kupigana na matifa hayo matatu,bali wao walimtegemea Bwana katika sifa na kuabudu huku wakisonga mbele za maadui zao ambao hao maadui walikuwa kwanza ni wengi pili walikuwa na silaha za kivita. Imeandikwa;
“ Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele.Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa.” 2 Mambo ya nyakati 20:21-22
Tazama hapo kwa makini; Hawa wakina Yuda ( Yehoshafati) walipoanza kuimba na kusifu,Bwana akaingilia vita hiyo naye Bwana akwapigania wakati akina Yuda wao wanaendelea tu kusonga mbele wakisifu na kumwimbia Bwana. Biblia inasema Bwana akaweka “waviziao” yaani watesi wakapigana wao kwa wao,ni kama vile walichanganyikiwa. Sijui kama unanielewa vizuri!
Si jambo jepesi hili,lakini inawezekana. Kumbe,vita si yetu bali ni ya Bwana,kwa maana Yeye Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki ( 1 Samweli 17:47 ) Lakini ni pale ambapo tunapokuwa tumejitoa kidhati kwa Bwana,naye Bwana hupigana mwenyewe.
Tatizo ulilonalo wewe mpendwa hutaki kujitoa kwa dhati kwa ajili ya BWANA ndio maana unatumia nguvu kubwa sana ya kupigana na maadui zako kwa sababu Bwana anakuwa hajausishwa. Akina Yehoshafati wasingeliweza kuwapiga maadui zao kama BWANA MUNGU asingehusishwa. Waweza kuniuliza Mungu alihusishwaje? Ni hivi;
Watu hawa kwanza waliomba,pili~Wakamsifu na kumuimbia Bwana Mungu katika uzuri wa utakatifu. Bwana akashuka na kuwashindia. Nikuulize swali moja; Je ni kweli katika ratiba zako,unatenga muda mzuri wa kumsifu Bwana na kumuabudu ? Kama la! Basi anza leo,hujachelewa.
Hata leo tunapitia vita nyingi sana,lakini ishu ni namna gani tunamtanguliza Bwana Mungu.
(III) MAOMBI YA TOBA NA REHEMA.
Bwana Yesu asifiwe…
Hii ni aina ya tatu ya maombi kwa mujibu wa mpangilio wangu nilioanza hapo mwanzo wa fundisho hili la undani wa maombi. Neno toba ni neno lenye asili ya kiyunani lenye maana ya geuka. Ndio maana tunapotubu ni sawa na kusema tunageuka kutoka dhambini na kumuelekea Mungu hivyo kutubu ni kumgeukia MUNGU. Mtu atubuye anahitaji rehema za Mungu.
Je nini tofauti kati ya toba na rehema?
~Toba ni tendo zima la kuungama dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha bali rehema ni huruma ya kiwango cha juu,(mara nyingine uhusishwa na msamaha). Pale unapotubia dhambi zako unahitaji kupokea huruma ya MUNGU kwamba akusamehe. Hivyo basi maneno haya mawili ingawa yanatofauti lakini hutumika pamoja.
Tunapojifunza aina hii ya maombi,lengo letu haswa ni kujua namna gani tunaweza kutumia toba na rehema katika maisha yetu ya kila siku. Ni ukweli kwamba tu wakosefu mbele za Mungu,lakini Mungu hupendezwa na yule anayetubu dhambi zake pale tu anapodondoka. ( Na isiwe mazoea kwamba ufanye dhambi ukitegemea kesho utatubu!!!)
Siku moja katika ibada zetu,mchungaji kiongozi aliuliza swali kwa kanisa zima ( haswa kwa wale waliokuwa wameokoka) kwamba;ni nani ambaye hajadanganya kabisa tangu alipookoka? Anyooshe mkono! Ukweli ni kwamba hakuna aliyenyoosha mkono hata mtu mmoja hapo kanisani. Hii ikiwa na maana kwamba wote tumeshawahi kudanganya mara nyingi katik wokovu wetu sijui wewe usomaye sasa hivi,je hujawahi kudanganya katika maisha yako ya wokovu?
Kumbe,mara nyingi tunafanya dhambi tena tunasahau kama tumetenda dhambi. Hatua ya kipekee itakayokuwezesha kukupa urejesho ni toba ya kweli (huku ukiwa umeokoka,kwa maana kuokoka hutangulia vyote).
Nataka uangalie jambo hili kwa mtazamo wa tofauti siku ya leo kwamba unahitaji kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi. Neno “kumaanisha kuacha dhambi” ni neno muhimu sana wakati wa kutubu.
Ni kweli nakubali kwamba hatuwezi kuacha dhambi kwa kutumia akili zetu za kibinadamu bali tunaweza kuacha dhambi na uovu wote kwa msaada wa Roho mtakatifu. Lakini ni lazima wewe mwenyewe uchukue hatua madhubuti ya kuamua kuacha dhambi huku ukimuomba Roho mtakatifu akusaidie.
Bwana Mungu hapendi mtu apotee bali sote tufikilie toba.( 2 Petro 3:9). Mungu hapendi wewe upotee katika dhambi hiyo uifanyayo mara kwa mara bali anataka leo ufikirie kutubu na kuamua kuacha. Haijarishi ni dhambi ya namna gani,kwa maana kwake MUNGU yote yanawezekana.
Yeye Mungu aweza kukuondolea leo hiyo kiu ya dhambi,maana anasema wale wote wenye kiu ya dhambi waende kwake naye ataikata kiu hiyo na kukupea kiu ya Kwake (Isaya 55:1-2)
Je nini haswa asili ya toba na rehema?
Asili ya toba ni pale dhambi ilipoingia ulimwenguni. Kwa maana twatubu kwa sababu ya uwepo wa dhambi. Hali ya kiroho ya mwanadamua wa kwanza kabla ya dhambi ilikuwa sawa na hali ya Mungu kwa maana wote walikuwa rohoni,lakini Mungu ni Mungu na mwanadamu ni mwanadamu kwa kuwa Mungu Yeye hakuumbwa bali mwanadamu aliumbwa. Baada ya dhambi kuingia ulimwenguni,mwanadamu akapoteza mfanano aliokuwa nao hapo awali (Mwanzo 3:9)
Je kutubu ni mpango wa MUNGU?
Ndio,Mungu ameachilia fursa ya kutubu kwetu. Kwa maana viumbe vingine havina nafasi hii,hata malaika hawana nafasi ya kutubu. Je unajua lusifa alipoasi tu,kilichofuata ni adhabu moja kwa moja? Hakukua nafasi ya toba kama tuliyokuwa nayo leo,hata akina Adam wangeliweza kutubia kuasi kwao.
Lakini hawakufanya hivyo na ndio maana BWANA MUNGU akamtuma mwanaye wa pekee ili kila amwaminiye awe na uzima wa milele (Yoh.3:16). Kazi ya Kristo Yesu ni kukomboa ulimwengu uliojaa dhambi (1 Timotheo 1:15). Kumbuka,nafasi hii ya toba haijaachiliwa kwa kusudi utende dhambi hivyo nafasi ya toba ni neema tu.
Watu wengi ulimwenguni leo wamekwama katika eneo la kutosamehewa dhambi zao kwa sababu ya wao wenyewe kushindwa kuwasamehe wakosa wao.( Mathayo 6:14-15) Hili ni tatizo kubwa sana,kwa maana ukiwa unatubu ni lazima ukumbuke kuwasamehe wengine kwanza na kuwaachilia kutoka moyoni kisha sasa ndio usamehewe na wewe. Usisahau hilo hata kidogo. Ukiwa una neno na nduguyo,patana naye kwanza kabla hujaenda madhabahuni.
Ikiwa umetubia dhambi lakini bado kila siku unairudia kuitenda hiyo hiyo,emu nipigie simu tuombe pamoja inawezekana tukaomba pamoja na ukatiwa nguvu ya ziada; piga kwa namba hii +255 655 11 11 49.
ITAENDELEA…
Mch.G.Madumla
Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)
S.L.P 55051.Dar. TZ.
UBARIKIWE.